TAKUKURU YAWATAKA WATUMISHI KUZINGATIA MAADILI, WANANCHI WAHIMIZWA KUTOA TAARIFA ZA RUSHWA


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga imezitaka taasisi za umma kutoa huduma kwa kuzingatia misingi ya maadili na uwajibikaji, hatua ambayo itasaidia kudhibiti vitendo vya rushwa.

Akitoa taarifa ya utendaji kwa kipindi cha robo mwaka kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga, Donacian Kessy, amesema kuzingatia maadili ni msingi muhimu wa kukomesha vitendo vya rushwa na kuboresha utoaji wa huduma.

Amesema katika kipindi hicho, TAKUKURU imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3 na kufanikiwa kuokoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 50, ikiwemo nondo, vigae, vifaa vya umeme na maji ambavyo havikuwasilishwa na mzabuni kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi katika Shule ya Msingi Magongwa Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama.

Kwa upande wa ukusanyaji mapato, taasisi hiyo imeimarisha udhibiti wa ukwepaji ushuru wa mazao katika Manispaa ya Shinyanga kupitia ufuatiliaji wa mifumo na doria maalum. Aidha, baada ya kutoa elimu ya maadili kwa watumishi wa afya wa Halmashauri ya Ushetu kufuatia malalamiko ya wananchi, mapato ya idara ya afya yameongezeka kutoka shilingi milioni 3 hadi milioni 14 kwa mwezi huku huduma zikiboreshwa.
Katika kipindi hicho, TAKUKURU imepokea malalamiko 39, yakiwemo 22 yanayohusu rushwa, ambapo kati ya kesi 4 zilizofunguliwa Mahakamani moja imetolewa uamuzi na  Jamhuri imeshinda kesi hiyo.

Kessy amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za viashiria vya rushwa kupitia namba ya simu ya bure.

PICHA WAKATI MKUU WA TAKUKURU MKOA WA SHINYANGA DONACIAN KESSY AKITOA TAARIFA YA ROBO MWAKA YA UTEKELEZAJI YA WA SHUGHULI MBELE YA WAANDISHI WA HABARI 














No comments

#tuandikie maoni yako.

Theme images by Storman. Powered by Blogger.