WANAOTEKELEZA AFUA ZA VVU NA UKIMWI WATAKIWA KUSHIRIKISHA NGAZI ZOTE
Maelekezo hayo yametolewa na Sekretarieti ya Mkoa inayoshughulikia masuala ya VVU na UKIMWI, kupitia kikao cha wadau wa utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI kilichofanyika leo, Machi 25, 2026, katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Katika kikao hicho, wadau wamepongezwa kwa mchango wao katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na VVU na UKIMWI.
Hata hivyo, wametakiwa kuimarisha utaratibu wa utoaji wa taarifa za utekelezaji wa shughuli zao kwa wasimamizi wa maeneo wanayofanyia kazi, wakiwemo waratibu wa kudhibiti UKIMWI ngazi ya jamii, hatua ambayo itaboresha usimamizi na ufuatiliaji wa miongozo iliyowekwa na Serikali.
Mwenyekiti wa kikao hicho Bi. Bestina Gunje amebainisha kuwa, bado kuna changamoto kwa baadhi ya mashirika kwenda moja kwa moja kwenye maeneo ya utekelezaji wa miradi bila kushirikisha mamlaka za eneo husika, kutokana na baadhi kuamini kuwa, hawawajibiki ngazi ya chini kwa sababu wamesajiliwa ngazi ya taifa.
Bi. Bestina Gunje, Mwenyekiti wa kikao na Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Shinyanga anayeshughulikia masuala ya MTAKUWWA
Bi. Gunje, ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga anayesimamia masuala ya MTAKUWWA, amesema kuwa hatua hiyo inakwamisha uelewa wa pamoja na uratibu mzuri wa shughuli, hivyo kudhoofisha juhudi za kushughulikia kwa pamoja changamoto zinazojitokeza.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Afua za VVU na UKIMWI, Mratibu wa kudhibiti UKIMWI ngazi ya jamii mkoa wa Shinyanga, Bi. Henrika Ignas, amesema pamoja na mafanikio yaliyopo, bado kuna viashiria vya unyanyapaa katika baadhi ya maeneo vinavyohitaji kuendelea kupatiwa ufumbuzi.

Mratibu wa UKIMWI ngazi ya jamii mkoa wa Shinyanga, Bi. Henrika Ignas
Kikao hicho ambacho kililenga kupata mrejesho na kujadili kwa pamoja namna bora ya kuimarisha utekelezaji wa mikakati ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, kimehudhuriwa pia na Mratibu wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Kanda ya Magharibi, Bw. Geofrey Mabu, anayesimamia mikoa ya Shinyanga, Tabora, Simiyu na Kigoma, ambaye alitilia mkazo maelekezo ya Sekretarieti ya mkoa.

Mratibu wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Kanda ya Magharibi, Bw. Geofrey Mabu,
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mratibu wa kudhibiti UKIMWI toka Idara ya Afya mkoa wa Shinyanga Dr. Peter Mlacha, Waratibu wa kudhibiti UKIMWI ngazi ya jamii kutoka Halmashauri mbalimbali za mkoa wa Shinyanga pamoja na wawakilishi wa mashirika yanayotekeleza Afua za VVU na UKIMWI katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga.
Zaidi ya mashirika 12 yanatekeleza afua za VVU na UKIMWI katika mkoa wa Shinyanga, ambayo ni pamoja na HUHESO Foundation, LOHADA, MUVUMA, Friends of Life Organization (FLO), Lifeline Counseling Center, Companion of Women and Children Empowerment (COWOCE), Fikra Mpya, TAYOA, Doctors with Africa (CUAMM), YAWE, KIWOHEDE, THPS na NACOPHA.
Picha za matukio mbalimbali katika kikao cha wadau wa Afua za VVU na UKIMWI mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye kikao
Post a Comment