ASKOFU SANGU AWATAKA MAPADRE KUWA KIELELEZO CHA IMANI

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu, amewataka Mapadre kuwa kielelezo cha imani kwa kumshuhudia Yesu Kristo kupitia maneno na matendo yao.

Rai hiyo ameitoa wakati akihubiri kwenye Misa ya Krisma iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Ngokolo mjini Shinyanga.

Misa hiyo iliambatana na Mapadre kurudia viapo vyao vya maisha ya wakfu.

Katika homilia yake, Askofu Sangu alibainisha kuwa Mapadre, kupitia daraja walilopokea, wana wajibu wa kuishi na kuishuhudia imani ya Kristo kwa maneno na matendo, huku wakiwaongoza waamini kutambua upendo, msamaha na huruma ya Mungu ili wamwongokee yeye.

Alisisitiza kuwa, Padre ataweza kuwa shahidi wa kweli wa imani endapo atakubali kuongozwa na Roho Mtakatifu katika maisha yake ya wakfu huku akionya kuwa, kinyume chake, anaweza kujikuta akijihubiria mwenyewe na kuwa chanzo cha changamoto mbalimbali, ikiwemo mateso kwa wengine, chuki, fitina na mafarakano.

Aidha, Askofu Sangu aliwakumbusha waamini kuwa, Mapadre kama wanadamu wengine, wanahitaji sala na maombezi ili waweze kupata nguvu ya kutimiza kwa uaminifu wito wao.

Katika Misa hiyo ya Krisma, pia kulifanyika ibada ya kuweka wakfu mafuta ya Krisma takatifu, kubariki mafuta ya wagonjwa na wakatekumeni, huku Mapadre wakirudia viapo vyao vya kipadre kama sehemu ya kuyafanya upya maisha yao ya wakfu.

Waamini pia waliwazawadia Mapadre wao ikiwa ni sehemu ya kuwategemeza na kuwatia moyo kutokana na huduma za kiroho wanazozitoa.

Kwa moyo wa upendo na majitoleo, Waamini wamewazawadia Mapadre wao zaidi ya Shilingi Milioni 600, huku Parokia ya Kanisa kuu Ngokolo ikiongoza kwa zawadi ya zaidi ya Shilingi Milioni 80, ikifuatiwa na Parokia ya Nyalikungu ambayo imetoa zaidi ya Shilingi Milioni 50 huku Parokia ya Lubaga ikiwa na zawadi zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 40.


No comments

#tuandikie maoni yako.

Theme images by Storman. Powered by Blogger.