SHINYANGA KUWA MWENYEJI WA MAONYESHO YA 5 YA SIDO KITAIFA
Mkoa wa Shinyanga utakuwa mwenyeji wa Maonyesho ya 5 ya SIDO ngazi ya kitaifa yatakayofanyika kuanzia Oktoba 21 hadi 30, 2026, katika Uwanja wa Magufuli uliopo Manispaa ya Kahama.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji,
amesema maonyesho hayo yatawakutanisha zaidi ya wajasiriamali na wazalishaji
600 kutoka Tanzania Bara na Visiwani, pamoja na taasisi zaidi ya 50 za serikali
na binafsi zinazohudumia sekta ya viwanda vidogo na vya kati.
Ameeleza
kuwa, maonyesho hayo yanalenga kutoa fursa kwa wajasiriamali kuonesha bidhaa na
teknolojia mbalimbali, kujifunza, kubadilishana uzoefu, kukuza ubunifu,
kuongeza thamani ya bidhaa, na kupanua masoko.
Vilevile yatasaidia kutangaza huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali zinawezesha wajasiliamali ambazo ni pamoja na Shirika la viwango Tanzania TBS na Wakala wa usajili na Leseni BRELA.

Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji
Aidha, Profesa Mpanduji ameyataja maonyesho hayo kuwa, yatakuwa fursa muhimu ya kuwajengea uwezo vijana, ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapa kipaumbele.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa (Utawala na Rasilimali Watu), David Lyamongi, amewahakikishia wadau kuwa mkoa wa Shinyanga umejipanga kikamilifu kuwa mwenyeji wa maonyesho hayo huku akiilezea Manispaa ya Kahama kuwa ni mji wa kibiashara unaokua kwa kasi, na una miundombinu yote inayofaa kwa ajili ya maonyesho hayo.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa (Utawala na Rasilimali Watu), David Lyamongi
Maonyesho hayo, yaliyoanza mwaka 2018, yanaratibiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la Maendeleo ya viwanda vidogo SIDO, kwa kushirikiana na TAMISEMI.


Post a Comment