ASKOFU SANGU KESHO KUWEKA WAKFU KRISMA TAKATIFU
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kesho Alhamisi tarehe 26,Machi 2026, ataweka wakfu mafuta ya Krisma takatifu kupitia adhimisho la Misa takatifu itakayofanyika katika Kanisa kuu la Mama mwenye Huruma Ngokolo, katika Manispaa ya Shinyanga.
Kwa mujibu
wa taarifa zilizotolewa na uongozi wa jimbo, Misa hiyo itaanza saa 4:00 asubuhi
na itahudhuriwa na Mapadre, watawa na waamini kutoka Parokia zote 23 za Jimbo la Shinyanga pamoja na Parokia teule
3 za Lyamidati, Mwakitolyo na Masanwa.
Kupitia Misa
hiyo, Askofu Sangu ataweka wakfu mafuta ya Krisma takatifu pamoja kubariki
mafuta ya wagonjwa na wakatekumeni mbapo pia Mapadre watarudia viapo vyao vya
maisha ya kipadre mbele ya Askofu na Kanisa, ikiwa ni sehemu ya kupyaisha
maisha yao ya wakfu na kuonyesha ushirika na Askofu wao.
Aidha, waamini watapata fursa ya kuwapongeza Mapadre wao kwa zawadi mbalimbali ikiwa ni hatua ya kuwatia moyo kutokana na huduma za kiroho wanazowapatia.Misa ya Krisma ni siku maalum ambayo imetengwa na Kanisa kwa ajili ya sherehe ya Mapadre
Misa ya Krisma ni siku maalum ambayo imetengwa na Kanisa kwa ajili ya sherehe ya Mapadre pamoja na kuweka wakfu mafuta ya Krisma takatifu, ambayo hutumika kwa shughuli mbalimbali za wakfu ikiwemo utolewaji wa daraja ya Upadre na Uaskofu, ubatizo, kipaimara pamoja na kutabaruku (kuweka wakfu)Kanisa na Altare.
Wakati huohuo, mafuta ya wagonjwa hutumika kwa ajili ya mpako wa wagonjwa huku mafuta ya wakatekumeni hutumika kuwapaka wanafunzi wa dini kwa ajili ya kuwaandaa kupokea Sakramenti ya Ubatizo.

Post a Comment