WIVU WA MAPENZI WAENDELEA KUGHARIMU MAISHA YA WANANDOA; POLISI YAMSAKA MSHUKIWA

Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Songambele, Kata ya Salawe katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, amefariki dunia kufuatia kile kinachodaiwa kuwa ni shambulio kutoka kwa aliyekuwa mume wake, likihusishwa na wivu wa mapenzi.

Tukio hilo limegundulika Jumatatu, Machi 23, 2026 majira ya saa moja asubuhi, ambapo mwanamke huyo aitwaye Mariam Cosmasi Mafumba (40), alikutwa amefariki dunia ndani ya nyumba yake katika mazingira ya kutatanisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha marehemu alipigwa kwa kitu kigumu sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwemo kichwani, kabla ya kupoteza maisha.

Ameeleza kuwa chanzo cha tukio hilo kinahisiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi, ambapo mtuhumiwa alimshuku marehemu kuwa na mahusiano na wanaume wengine.

Kamanda Magomi amelielezea tukio hilo kuwa ni la kikatili na kusema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi, ikiwa ni pamoja na juhudi za kumtafuta mtuhumiwa aliyetajwa kwa jina la Manyanda Mbuye, anayedaiwa kuwa mume wa marehemu.

Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Songambele, Lazaro Enock, alieleza kuwa kabla ya kifo chake, Mariam alikuwa na mgogoro wa kifamilia na mume wake, uliyekuwa akimtuhumu kuishi na mwanaume mwingine aliyemtambulisha kama ndugu yake, ingawa baadaye ilibainika kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, watoto wa marehemu walidai kuwa mwanaume huyo ambaye alikuwa ameondoka na kubeba vitu vyake, siku ya tukio alifika nyumbani usiku na kuwataka waende kulala mapema na walipoamka asubuhi, walimkuta mama yao akiwa amefariki dunia.

 

No comments

#tuandikie maoni yako.

Theme images by Storman. Powered by Blogger.