WAKRISTO WAKUMBUSHWA KUWAJALI WENYE UHITAJI
Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, wameombwa kwa namna ya pekee kuguswa na kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali, wakiwemo, yatima, wafungwa na wazee wasiojiweza.
Mwaliko huo umetolewa na Mkurugenzi wa utume wa CARITAS wa Jimbo Katoliki Shinyanga Padre Charles Mashimbe, wakati akitoa tafakari kuhusu nafasi ya waamini na watu wote katika Jumapili ya Msamaria mwema, inayoadhimishwa na Kanisa Katoliki kote ulimwenguni kila Jumapili ya kwanza ya mwezi Septemba.
Padre Mashimbe amebinisha kuwa, katika maadhimisho ya siku ya Msamaria mwema, Kanisa huhamasisha moyo wa huruma na upendo kwa watu wenye shida mbalimbali, likifuata mafundisho ya Kristo aliyoyatoa kupitia mfano wa mtu msamaria aliyemtendea wema mtu myahudi ambaye walikuwa hawafungamani naye, akinukuu Injili ya Luka Sura 10, aya ya 29 hadi 37 (10:29-37)
Kupitia tafakari hiyo, Padre Mashimbe amewaomba wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa, kuwajali na kuwasaidia watu walioko kwenye mazingira magumu na duni, kadiri ya mahitaji yao, ili na wao waonje huruma, ukarimu na upendo wa Mungu, kupitia baraka ambazo amewajalia wanadamu.
Amesema katika jimbo la Shinyanga CARITAS imeweka utaratibu maalum wa kijimbo kuwasaidia wahitaji walioko kwenye mazingira yanayoonekana kama vile wafungwa walioko kwenye Magereza ya Mhumbu mjini Shinyanga, Maswa na Malya mkoani Simiyu, wazee wasiojiweza walioko kwenye vituo vya Kolandoto na Usanda pamoja na watoto wenye Ualbino wanaolelewa katika kituo cha Buhangija mjini Shinyanga, kwa kuwachangia kitu chochote ikiwemo, nguo, fedha, chakula na mahitaji mengine.
Padre Mashimbe ameelekeza kuwa, misaada hiyo ikusanywe kuanzia ngazi ya Jumuiya mpaka Parokia kwa kushirikiana na Maparoko, ambapo baadaye itakusanywa pamoja kwenye Ofisi ya CARITAS na kupelekwa kwa walengwa.
Post a Comment