RAFIKI SDO YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA KWA MJADALA, WATOTO WATOA USHAURI KWA WZAZI NA JAMII

Shirika la kutetea haki za vijana, wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalum la RAFIKI SDO, leo jumanne tarehe 16, Juni, 2026, limeadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kuandaa mjadala maalum uliowakutanisha watoto na wadau mbalimbali kujadili haki, ustawi na maendeleo ya watoto.

Mjadala huo uliofanyika  katika makao makuu ya shirika hilo yaliyopo Kata ya Kitangili, Manispaa ya Shinyanga, ambao uliongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Manispaa ya Shinyanga, Noelina Nicolaus Busisi.

Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Manispaa ya Shinyanga, Noelina Nicolaus Busisi.

Watoto walioshiriki mjadala huo walisisitiza umuhimu wa malezi bora, mazingira salama na fursa sawa kwa watoto wa kike na wa kiume.

Watoto hao pia waliomba kuimarishwa kwa elimu ya afya ya uzazi ili kuwasaidia kujitambua na kujikinga dhidi ya changamoto mbalimbali zinazotokana na kutokuwa na elimu hiyo,  ambazo ni pamoja na mimba za utotoni, ndoa za mapema na maambukizi ya magonjwa ya zinaa.

Aidha, watoto walieleza wasiwasi wao kuhusu matumizi yasiyodhibitiwa ya simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki, wakitaka wazazi na walezi kuongeza usimamizi ili kuwalinda dhidi ya athari za matumizi mabaya ya teknolojia.

Mbali na maoni hayo ya watoto, washiriki wote wa mjadala huo walijadili changamoto ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na hasa katika Kata ya Kitangili, ambapo waliweka mikakati mbalimbali ya  kukabiliana na hali hiyo.

Baadhi ya mikakati iliyopendekezwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano, semina na kampeni za uhamasishaji kuhusu malezi bora na ulinzi wa watoto, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, wazazi, viongozi wa jamii na wadau wa maendeleo katika kubaini mapema na kushughulikia changamoto zinazowakabili watoto hao.

Akifungua mjadala huo, Mkurugenzi wa RAFIKI SDO, Gerald Ng’ong’a, alipongeza juhudi za Serikali katika kulinda haki za watoto kupitia utekelezaji wa sera mbalimbali, ikiwemo sera ya elimu bila malipo na uanzishwaji wa mabaraza ya watoto yanayowapa nafasi ya kusikika na kutetea haki za wenzao.

Alisema RAFIKI SDO itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kutoa elimu kwa jamii, kuokoa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuhakikisha wazazi na walezi wanatekeleza wajibu wao wa malezi.

Akihitimisha mjadala huo, Diwani wa Viti Maalum katika Manispaa ya Shinyanga, Moshi Kanje, aliwataka wadau wote kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na watoto ili kuhakikisha wanakua katika mazingira salama na yanayowawezesha kufikia ndoto zao.

Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka Juni 16 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa Soweto nchini Afrika Kusini waliouawa na kujeruhiwa mwaka 1976 walipokuwa wakidai haki ya kupata elimu bora. Maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha jamii, serikali na wadau mbalimbali kuendelea kulinda na kutetea haki za watoto barani Afrika

Mratibu wa Baraza la watoto wa Manispaa ya Shinyanga Bi.Kashinje Shija (mwenye vazi la Zambarau) akiwa kwenye mjadala wa watoto na Afisa Maendeleo ya jamii wa Kata ya Kitangili Bi. Kabula Shija (mwenye vazi la kijani)

Diwani wa Viti maalum Manispaa ya Shinyanga Mh.Moshi Kanje akizungumza kwenye mjadala wa siku ya mtoto wa Afrika

Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI SDO Bw. Gerald Ng'ong'a akizungumza na wadau wakiwemo watoto kwenye mjadala 



Bw. Gerald Ng'ong'a akizungumza na watoto baada ya mjadala kuanza

Mkuu wa dawati la jinsia  kutoka Jeshi la Polisi Wilaya ya Shinyanga Mkaguzi wa Polisi Jane Mwazembe akichangia jambo kwenye mjadala
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kitangili Bi.Linda Kibirige akipokea maoni ya wadau ya namna ya kushirikiana katika kudhibiti watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwenye Kata yake
Mwakilishi wa umoja wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayojihusisha na kudhibiti ukatili kwa wanawake na watoto katika mkoa wa Shinyanga, ambaye pia ni Diwani wa viti maalum Mh.Veronica Massawe, akitoa maoni ya namna ya kudhibiti hali ya watoto kuishi katika mazingira hatarishi

Wawakilishi wa watoto wakiwa kwenye picha ya pamoja na wadau walioshiriki mjadala

Watoto wakitoa maoni mbalimbali kwenye mjadala




No comments

#tuandikie maoni yako.

Theme images by Storman. Powered by Blogger.