MAPADRI WAWILI AMBAO NI WANAHABARI WABOBEVU WACHAGULIWA KUONGOZA SIGNIS DUNIANI NA AFRIKA
Na ANATOLI Salawa.
Mapadri wawili ambao ni wanahabari wambobevu wamechaguliwa kushika nafasi za juu za uongozi wa SIGNIS, shirika la kimataifa linalosimamia masuala ya habari na mawasiliano katika Kanisa Katoliki ulimwenguni.
Uchaguzi huo umefanyika wakati wa kilele cha Kongamano la
Kimataifa la SIGNIS lililoanza Agosti 3, 2026, na kuhitimishwa mwishoni mwa
wiki jijini Kigali, Rwanda, likiwakutanisha zaidi ya wanahabari 260 kutoka
sehemu mbalimbali duniani.
Waliochaguliwa ni Padri Profesa Walter Chikwendu
Ihejirika kutoka Nigeria, ambaye amechaguliwa kuwa Rais wa SIGNIS
Ulimwenguni, huku Padri Fedele Mutabazi kutoka Rwanda akichaguliwa kuwa
Rais wa SIGNIS Barani Afrika.
Kabla ya kuchaguliwa kuongoza SIGNIS Ulimwenguni, Profesa
Ihejirika alikuwa Rais wa SIGNIS Barani Afrika, nafasi ambayo aliitumikia kwa
ufanisi mkubwa akitumia uzoefu wake katika tasnia ya habari na mawasiliano.
Profesa Ihejirika pia alikuwa miongoni mwa viongozi
walioshiriki kikamilifu katika maandalizi ya Kongamano la Kimataifa la SIGNIS
lililofanyika jijini Kigali, ambalo lilihitimishwa kwa mafanikio makubwa baada
ya washiriki kujadili kwa kina nafasi ya vyombo vya habari na mawasiliano
katika kueneza ujumbe wa Kanisa, kuimarisha maadili ya uandishi wa habari na kutumia
fursa za maendeleo ya teknolojia kuwafikia watu ili kujenga umoja, amani na
mshikamano katika jamii.
Kwa upande wake, Padri Fedele Mutabazi alikuwa
Katibu Mtendaji wa Tume ya Upashanaji Habari katika Baraza la Maaskofu Katoliki
nchini Rwanda kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa SIGNIS Barani Afrika.
Kuchaguliwa kwa viongozi hao kunatarajiwa kuimarisha nafasi ya SIGNIS katika kuendeleza matumizi ya habari na mawasiliano kama nyenzo muhimu ya uinjilishaji, elimu, mawasiliano na kujenga jamii yenye mshikamano.

Post a Comment