RC MHITA AWATAKA WAZAZI NA WALEZI KUJITOKEZA KATIKA AWAMU YA PILI YA CHANJO YA POLIO

 

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amewataka wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi kwenye awamu ya pili ya chanjo ya Polio, inayotarajiwa kuanza kutolewa  kesho kwa watoto wa chini ya miaka 10 katika maeneo yote ya mkoa.

Akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake, Mhita amesema chanjo hiyo ya awamu ya pili, itatolewa kwa siku nne kuanzia kesho Alhamisi tarehe 07 hadi Jumapili tarehe 10, Mei, 2026 , ikiwa na lengo la kukamilisha dozi ya chanjo iliyotolewa Machi 24 hadi 27,mwaka huu 2026.

Amesisitiza kila mzazi na mlezi kuhakikisha mtoto wake anapata chanjo hiyo na kuwapa ushirikiano wataalam wa afya watakaokuwa wakitekeleza zoezi hilo, ili kuwakinga watoto na ugonjwa wa Polio ambao ni hatari kwa afya zao.

Mhita amebainisha kuwa, Chanjo hiyo ya matone ya Polio, itatolewa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya, shuleni na nyumba kwa nyumba na anatarajia  zoezi hilo litafanikiwa kwa kiwango kinachotakiwa kama ilivyokuwa kwa awamu ya kwanza  ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi.

Amewataka wananchi kuacha kusikiliza  upotoshaji dhidi ya dhamira njema ya Serikali katika kulinda afya za wananchi hususani watoto.

Mhita pia amempongeza Rais Dkt. Samia suluhu Hassan kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya Afya, ambapo mkoa wa Shinyanga umenufaika katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vipya vya afya, Hospitali na zahanati, ununuzi wa vifaa tiba, ongezeko la watumishi kupitia ajira mpya, pamoja na madaktari wa mkoa wa Shinyanga kupata fursa ya kwenda kuongeza elimu na kuwa madaktari bingwa, hatua ambayo   imeboresha kwa kiwango kikubwa utoaji wa huduma za afya.

Mratibu wa Elimu ya Afya kwa umma wa mkoa wa Shinyanga Moses Mwita akiwa kwenye Kikao cha waandishi wa Habari na mkuu wa mkoa kilichohusu awamu ya pili ya chanjo ya Polio

No comments

#tuandikie maoni yako.

Theme images by Storman. Powered by Blogger.