MADIWANI SHINYANGA WAOMBWA KUWA NA SUBIRA WAKATI SUALA LA USHURU WA WACHIMBAJI LIKIFANYIWA TATHMINI

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Seth Antony Msangwa 

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wameombwa kuwa na subira wakati Ofisi ya Mkurugenzi ikiendelea kushughulikia changamoto ya ushuru wa mchanga na mawe kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kata ya Mwakitolyo.

Hoja hiyo ilitolewa kwenye Kikao cha baraza la Madiwani na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mheshimiwa Seth Antony Msangwa, kufuatia swali la Diwani wa Kata ya Mwakitolyo, Masalu Nyese Lusana, alilouliza katika kikao cha kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Kata, kilichofanyika leo Jumanne tarehe 05, Mei, 2026, katika Ukumbi wa Halmashauri. 

 Diwani huyo alitaka kujua ni lini tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi, akieleza kuwa limesababisha kusimama kwa shughuli za uchimbaji na hivyo kuathiri mapato ya Halmashauri na uchumi wa wananchi.

Diwani wa Kata ya Mwakitolyo Mh. Masalu Nyese Lusana

Kufuatia hoja hiyo, Mwenyekiti huyo aliwataka madiwani kuwa wavumilivu ili kuipa nafasi timu maalum ya wataalamu iliyoundwa na Mkurugenzi kufanya tathmini ya kina kuhusu suala hilo.

Alibainisha kuwa taarifa ya uchunguzi huo itawasilishwa na kujadiliwa katika Baraza la Madiwani.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Joseph Ntomela, alisema tayari ofisi yake imeunda timu ya kuchunguza changamoto hiyo, na kwamba baada ya kukamilika kwa uchunguzi, watawasilisha mapendekezo kwa madiwani ili kupata suluhisho la kudumu.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Joseph Ntomela

Chanzo cha mzozo huo kinatajwa kuwa ni sheria ndogo iliyotungwa na Halmashauri inayotoza ushuru wa shilingi laki mbili kwa kila gari linalobeba mchanga au mawe kutoka kwenye vitalu vya uchimbaji vinavyomilikiwa na vikundi vya wananchi, bila kuzingatia thamani halisi ya mzigo.

Hatua hiyo imelalamikiwa na wachimbaji wadogo, wakidai kuwa wanabebeshwa gharama kubwa zikiwemo ushuru wa huduma na kodi nyingine, hali iliyosababisha kusitishwa kwa muda kwa shughuli za uchimbaji na kuathiri uchumi wa eneo hilo.

Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo alimtaka Mkurugenzi, kwa kushirikiana na wataalamu wake, kuandaa majibu ya kina kuhusu changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na madiwani, kwa ajili ya kikao kijacho.

Naye Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, Bw. Omary Mwenda, aliwapongeza madiwani kwa uwajibikaji wao katika kuwasimamia wataalamu na kuwakilisha wananchi, huku akiwahimiza kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi sahihi ya fedha za Serikali.

Wakuu wa Idara na watalaam wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani
Madiwani wakiwa kwenye kikao

 


No comments

#tuandikie maoni yako.

Theme images by Storman. Powered by Blogger.