MIAKA 11 YA ASKOFU SANGU: CHIMBUKO LA JIMBO JIPYA LA BARIADI NA MAGEUZI YA KIROHO NA KIJAMII SHINYANGA
Askofu Liberatus Sangu, kesho Jumapili tarehe 12 Aprili 2026, anamshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 11 ya Uaskofu na utume katika Jimbo la Shinyanga.
Alizaliwa tarehe 19 Februari 1963 katika Kijiji cha Mwanzye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Alipata malezi ya kikasisi katika Seminari Kuu za Kibosho (Moshi) na Segerea (Dar es Salaam), ambako alipewa mafunzo ya falsafa na teolojia.
Alipadrishwa
tarehe 3 Julai 1994 katika Jimbo la Sumbawanga na kuanza utume wake kwa
kuhudumu katika nafasi mbalimbali, ikiwemo ulezi wa seminari, uparoko na
uongozi wa miito. Kuanzia mwaka 1996 hadi 1999 alijiendeleza kielimu mjini
Roma, Italia, na kupata Shahada ya Uzamili katika taaluma ya Sakramenti za
Kanisa.
Baadaye
aliteuliwa kufanya kazi Vatican kama Afisa Mwandamizi katika Idara ya
Uinjilishaji wa Watu, ambako alipata uzoefu mkubwa wa utume wa Kanisa kimataifa.
Mwanzo wa
Utume na Msingi wa Uongozi
Katika historia ya Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, uongozi wa Askofu Sangu umebeba sura ya mageuzi makubwa ya kiroho, kijamii na kiutawala.
Anapotimiza
miaka 11 tangu kuwekwa wakfu na kusimikwa kwake kuwa Askofu wa nne wa Jimbo
hilo, mchango wake umeacha alama isiyofutika, ikiwemo kuzaliwa kwa Jimbo jipya la
Bariadi.
Askofu Sangu
aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Shinyanga tarehe 2 Februari 2015 na Hayati
Baba Mtakatifu Fransisko, kufuatia kifo cha mtangulizi wake Askofu Aloysius
Balina kilichotokea Novemba 6, 2012.
Aliwekwa
wakfu na kusimikwa rasmi Aprili 12, 2015, akitokea Vatican ambako alikuwa
akihudumu katika Idara ya Uinjilishaji wa Watu.
Akiwa na
kaulimbiu isemayo “Tunda la roho ni upendo”, alianza utume wake kwa
dhamira ya kuimarisha imani, kuendeleza mshikamano wa waamini na kulijenga
Kanisa linalojitegemea.
Moja ya misingi mikuu ya uongozi wake imekuwa ni kusogeza huduma za kiroho karibu na waamini, hasa walioko maeneo ya pembezoni.
Kupitia mkakati huu, alifanya ziara nyingi katika maeneo yaliyokuwa hayafikiki kwa urahisi kutokana na changamoto za miundombinu na umbali.
Matokeo ya juhudi hizo ni ongezeko la Parokia kutoka 26 alizozikuta hadi kufikia 40, baada ya kuanzisha Parokia mpya 14. Hatua hii imeimarisha huduma za kichungaji na kuwafikia waamini wengi zaidi, hususan katika maeneo ya vijijini.
Chimbuko
la Jimbo Jipya la Bariadi
Katika
kuendeleza dhana ya kusogeza huduma, Askofu Sangu alianzisha mchakato wa
kugawanywa kwa Jimbo la Shinyanga ili kuunda Jimbo jipya la Bariadi. Hatua hiyo
ililenga kuwapa waamini huduma za karibu zaidi na uongozi unaowafikia kwa
urahisi.
Hatimaye, tarehe 19 Machi 2026, Jimbo la Bariadi lilizinduliwa rasmi, na kumpata Askofu wake wa kwanza Mhashamu Prosper Baltazar Lyimo, likiwa ni moja ya mafanikio makubwa ya kihistoria katika kipindi cha uongozi wa Askofu Sangu.
Ikumbukwe kwamba, baada ya Jimbo la Shinyanga kuzaa Jimbo jipya la Bariadi kwa sasa limebaki na Parokia 24 na Parokia teule tatu za Masanwa, Mwakitolyo na Lyamidati ambazo zimewekewa Mapadri wa kuzihudumia.

Kuimarisha
Miito na Rasilimali Watu
Katika kuhakikisha huduma za Kanisa zinaendelea, Askofu Sangu alitoa msukumo mkubwa kwa vijana kuitikia wito wa upadre na utawa. Idadi ya waseminari iliongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka chini ya 10 hadi zaidi ya 70, huku wengi wao tayari wakiwa Mapadre wanaohudumu ndani na nje ya Jimbo ikiwemo Jimbo jipya la Bariadi na wengine wakiendelea na masomo ya majiundo ya kipadri kwenye Seminari mbalimbali nchini.
Aidha,
amewezesha Mapadri zaidi ya 20 kujiendeleza kielimu ndani na nje ya nchi, hatua
iliyoongeza ubora wa huduma za kichungaji na kitaaluma.
Kuendeleza
Elimu na Afya
Akitekeleza
dhana ya kumhudumia binadamu mzima—mwili na roho—Askofu Sangu amewekeza katika
sekta za elimu na afya. Ameanzisha na kuimarisha shule za msingi na sekondari,
huku akisisitiza kila Parokia kuwa na eneo la elimu, hasa kwa watoto wadogo.
Kwa upande wa afya, ameendeleza huduma kupitia zahanati, vituo vya afya na hospitali, akishirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha huduma hizo kwa jamii bila ubaguzi.
Mafanikio
ya Seminari na Malezi ya Vijana
Seminari
Ndogo ya Shanwa iliyopo Maswa imepata mafanikio makubwa chini ya uongozi wake,
ikiboreshwa miundombinu na ubora wa ufundishaji. Kwa sasa, seminari hiyo licha
ya kupokea wanafunzi kutoka Jimbo la Shinyanga, pia inapokea wanafunzi kutoka
majimbo mbalimbali ikiwemo Jimbo kuu la Mwanza, Jimbo la Geita, Jimbo la
Musoma, Jimbo la Bunda na Jimbo jipya la Bariadi na imekuwa miongoni mwa shule
zinazofanya vizuri kitaaluma katika Mkoa wa Simiyu.
Vilevile,
ameimarisha malezi ya vijana kupitia vyama vya kitume, akilenga kuwajenga
kiimani, kimaadili na kijamii.
Huduma za
Kijamii na Mawasiliano
Katika
upande wa huduma za kijamii, Askofu Sangu alifufua na kuimarisha shirika la
CARITAS, linalowasaidia watu wenye uhitaji kwa kuwawezesha kiuchumi na kijamii.
Aidha, amewekeza katika kuboresha miundombinu ya Redio Faraja ili iwe chombo madhubuti cha kuelimisha, kuhabarisha na kuunganisha jamii. Redio hiyo pia imekuwa jukwaa la kukuza mshikamano wa kidini kwa kutoa nafasi kwa madhehebu mbalimbali

Kukuza
Umoja, Amani na Maadili
Katika mafundisho yake, Askofu Sangu amesisitiza umuhimu wa amani, upendo na mshikamano, huku akipinga vikali vitendo vya ubinafsi, ukatili dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na migawanyiko ya kijamii.Ameendelea kuwa sauti ya maadili mema, akihimiza jamii kuishi kwa kuzingatia utu, haki na mshikamano.
Hitimisho
Miaka 11 ya uongozi wa Askofu Liberatus Sangu imeleta mageuzi makubwa ndani ya Jimbo la Shinyanga. Kuanzia kuimarisha imani ya waamini, kuongeza miundombinu ya Kanisa, kukuza rasilimali watu hadi kuanzishwa kwa Jimbo jipya la Bariadi—yote haya yanadhihirisha uongozi wenye dira na matokeo chanya.
Hayo yote amekuwa akiyataja kuwa yamewezekana kwa uwezo na nguvu za Mwenyezi Mungu, na anayepaswa kupewa sifa na utukufu ni Mungu mwenyewe

Mungu amjalie maixha mrefu
ReplyDelete